Aya
60
Mahali iliteremshwa
Makka
SURAT ADH-DHAARIYAAT
(Imeteremka Makka)
Sura hii imeanza kwa kiapo cha ukweli wa kufufuliwa na kutokea malipo. Kisha ikafuatisha kwa kiapo kingine juu ya ubabaishi wa wanao kanya katika maneno yao juu ya Mtume Wa Mwenyezi Mungu, na juu ya Qur'ani tukufu Kisha ikaingia kuwaonya wanao kanya kuwa watapata mwisho muovu katika Akhera. Tena ikaeleza waliyo ahidiwa wachamngu katika malipo ya vitendo vyao vyema walivyo vitanguliza duniani. Kisha kawazindua watu wazingatie Ishara za Mwenyezi Mungu katika kuumba kwake, na katika nafsi zao, na katika mambo ya ufundi wa ajabu na uzuri wa umbo alio uweka humo.
Na ikasimulia kisa cha Ibrahim na wageni wake Malaika, kisha ikaeleza hali za baadhi ya mataifa na maangamizo yaliyo wasibu kwa kuwakadhibisha Manabii wao. Kisha ikaashiria kwa jumla baadhi ya Ishara za uumbaji, na ikahimiza watu warejee kwa Mwenyezi Mungu, na wamuabudu Yeye peke yake, ambayo hayo ndio makusudi ya kuumbwa majini na watu. Na Sura imekhitimisha kwa kuwaonya wanao mkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. kuwa watapata adhabu iliyo kwisha wapata kaumu za kabla yao.