Sura An-Nisaa

Aya

176

Mahali iliteremshwa

Madina

Kipindi cha Kuteremshwa

Sura hii ina mijadala kadhaa ambayo iliteremshwa katika nyakati tofauti ima katika kipindi kati ya mwisho wa mwaka wa 3 na mwisho wa mwaka wa 4 au mwanzo wa mwaka wa 5 baada ya Hijra. Ingawa ni vigumu kubaini tarehe halisi ya kuteremshwa kwake, inawezekana kufanya makadirio ya kipindi sahihi tukizingatia amri zilizotolewa katika Sura na matukio yaliyotajwa humo, pamoja na Hadithi zilizohusishwa. Mifano michache imetolewa hapa chini:

  1. Tunajua kwamba maagizo kuhusu mgawanyo wa urithi wa mashahidi na kwa ajili ya kulinda haki za mayatima yalitumwa baada ya Vita vya Uhud ambapo Waislamu 70 waliuawa.Baada ya tukio hilo, swali la urithi na ulinzi wa mayatima lilijitokeza katika familia nyingi za Al-Madina. Kutokana na muktadha huu, tunaweza kuhitimisha kwamba Aya 1–28 ziliteremshwa wakati huo.
  2. Tunajifunza kutokana na Hadithi kwamba Amri kuhusu sala wakati wa vita ilitolewa wakati wa Zat-ur-Riqa'a, msafara uliofanyika mwaka wa 4 H. Kutokana na ushahidi huu, tunaweza kuhitimisha kwamba aya 102 iliteremshwa katika kipindi hicho.
  3. Onyo la mwisho (Katika aya ya 47) kwa Wayahudi lilitolewa kabla ya Banu Nadir kufukuzwa kutoka Al-Madinah katika mwezi wa Rabi‘-ul-Awwal, mwaka wa 4 H. Kwa msingi huu, inaweza kuhitimishwa kwa usalama kwamba aya ya 47 iliteremshwa muda mfupi kabla ya tukio hilo.
  4. Ruhusa ya tayammum (kutawadha kwa kutumia vumbi safi iwapo maji hayapatikani) ilitolewa katika msafara wa Bani al-Mustaliq, uliofanyika mwaka wa 5 H. Kwa msingi huu, inaonekana kwamba aya ya 43 iliteremshwa katika kipindi hicho.
  5.  

Mada na Msingi Wake

Hebu sasa tuchunguze mazingira ya kijamii na kihistoria ya kipindi hicho ili kuielewa Sura. Mazungumzo yote katika Sura hii yanashughulikia matatizo matatu makuu yaliyomkabili Mtume Mtukufu wakati huo. Kwanza kabisa, alikuwa akihusika katika kuleta maendeleo ya Jumuiya ya Kiislamu ambayo yalikuwa yameanzishwa wakati wa kuhamia kwake Al-Madina. Kwa kusudi hili, alikuwa akiweka misingi mipya za kimaadili, kitamaduni, kijamii, kiuchumi, na kisiasa badala ya desturii za kipindi cha kabla ya Uislamu. Changamoto ya pili iliyohitaji umakini na juhudi zake lilikuwa mapambano makali yaliyoendelea na Waarabu washirikina, koo tofauti za Kiyahudi, na wanafiki waliokuwa wakipingana na dhamira yake ya mageuzi. Zaidi ya hayo, ilibidi aeneze Uislamu mbele ya upinzani mkali wa nguvu hizi za uovu kwa lengo la kushinda akili na mioyo za watu.

Kwa hivyo, maagizo ya kina yametolewa kwa ajili ya kuimarisha na kuidumisha Jumuiya ya Kiislamu katika mwendelezo wa yale yaliyotolewa katika Al-Baqarah. Kanuni za uendeshaji bora wa maisha ya familia zimewekwa na njia za kutatua migogoro ya kifamilia zimefundishwa. Sheria zimeagizwa kwa ajili ya ndoa na haki za mke na mume zimegawanywa kwa haki na usawa. Hadhi ya wanawake katika jamii imebainishwa, tamko la haki za yatima limefanywa kuwa sheria, na kanuni zimewekwa kwa ajili ya mgawanyo wa mirathi, huku maagizo yakitolewa ya kurekebisha masuala ya kiuchumi. Msingi wa kanuni ya adhabu umewekwa, unywaji pombe umepigwa marufuku, na maagizo yametolewa kwa ajili ya usafi na tahara. Waislamu wamefundishwa aina ya mahusiano ambayo waumini wema wanapaswa kuwa nayo na Mwenyezi Mungu wao pamoja na wenzao. Aidha, maelekezo yametolewa kwa ajili ya kudumisha nidhamu ndani ya Jumuiya ya Kiislamu.

Hali ya maadili na kidini ya watu wa Kitabu imepitiwa upya ili kuwafundisha Waislamu masomo na kuwaonya mapema wajiepushe na kufuata nyayo zao. Mwenendo wa wanafiki umekosolewa, na sifa za unafiki pamoja na alama za imani ya kweli zimeainishwa kwa uwazi ili kuwawezesha Waislamu kutambua tofauti kati ya hizo.

Ili kukabiliana na matokeo ya Vita vya Uhud, maelekezo yenye kutia moyo yaliteremshwa ili kuwahimiza Waislamu wakabiliane na adui kwa ushujaa, kwani kushindwa katika vita hivyo kuliwapa koo za Waarabu washirikina, Wayahudi wa jirani, na wanafiki wa nyumbani ujasiri kiasi cha kuwatishia Waislamu kutoka pande zote. Katika hatua hii muhimu, Mwenyezi Mungu aliwajaza Waislamu ujasiri na kuwapa maagizo yaliyohitajika wakiwa katika hali ya vita. Ili kukabiliana na uvumi wa kutisha uliokuwa ukienezwa na wanafiki na Waislamu wa imani dhaifu, waliagizwa kufanya uchunguzi wa kina na kuwafahamisha wenye jukumu kuhusu hali yao. Aidha, walikabiliwa na matatizo ya kuswali wakati wa safari katika maeneo yenye ukosefu wa maji ya kutolea wudhuu. Katika hali kama hizo, waliruhusiwa kujisafisha kwa udongo safi, kufupisha swala, au kuswali “Swala ya Hofu” walipokabiliwa na hatari. Maagizo pia yalitolewa kwa ajili ya suluhisho la tatizo la Waislamu waliokuwa wametawanyika miongoni mwa koo za Kiarabu wasioamini na mara nyingi walihusika katika vita, ambapo waliombwa kuhamia Al-Madinah, makao ya Uislamu.

Sura hii pia inasimulia kisa cha Bani Nadir ambao walikuwa wakionyesha tabia ya uadui na ya kutisha, licha ya mikataba ya amani waliyoifanya na Waislamu. Walikuwa wakiunga mkono waziwazi maadui wa Uislamu na kupanga njama dhidi ya  Mtume mtukufu na Jumuiya ya Waislamu hata huko Al-Madinah yenyewe. Walichukuliwa hatua kwa tabia yao ya uadui na kupewa onyo la mwisho la kubadilisha mtazamo wao na hatimaye walifukuzwa kutoka Al-Madinah kwa sababu ya utovu wao wa nidhamu.

Tatizo la wanafiki, ambao wakati huo walikuwa wameanza kuwa wasumbufu sana, lilikuwa likiwatia Waumini katika mashaka makubwa. Kwa hiyo, waligawanywa katika makundi tofauti ili kuwawezesha Waislamu kuwashughulikia kwa njia inayofaa.

Maagizo ya wazi pia yalitolewa kuhusu mtazamo wanaopaswa kuufuata kuelekea koo ambazo hazikupigana vita. Jambo muhimu zaidi lililohitajika wakati huo lilikuwa kuwaandaa Waislamu kwa mapambano makali dhidi ya wapinzani wa Uislamu. Kwa kusudi hili, umuhimu mkubwa uliwekwa katika malezi ya tabia zao, kwani ilikuwa dhahiri kwamba Jumuiya ndogo ya Waislamu ingeweza kufanikiwa, au hata kuendelea kuishi, iwapo tu wangejengeka kwa tabia bora za kimaadili. Hivyo basi, waliamriwa kujipamba kwa sifa njema za maadili, na walikosolewa vikali kila udhaifu wa kimaadili ulipobainika ndani yao.

Ingawa Sura hii inashughulikia hasa mageuzi ya maadili na kijamii, umakini mkubwa pia umeelekezwa katika uenezaji wa Uislamu. Kwa upande mmoja, ubora wa maadili na utamaduni wa Kiislamu umeanzishwa juu ya ule wa Wayahudi, Wakristo, na Mushriki; kwa upande mwingine, dhana zao potofu za kidini, maadili yao potofu, na matendo yao maovu yamekosolewa ili kuandaa msingi wa kuwaalika kwenye njia ya Ukweli.

Mada: Kuimarisha Jumuiya ya Kiislamu

Lengo kuu la Sura hii ni kuwafundisha Waislamu njia zinazowaunganisha watu na kuwafanya wawe imara na wenye nguvu. Utangulizi kuhusu utulivu wa familia, ambao ndio kiini cha jamii umetolewa. Kisha wamehimizwa kujiandaa kwa ajili ya ulinzi. Sambamba na haya, wamefundishwa umuhimu wa uenezaji wa Uislamu. Zaidi ya yote, msisitizo mkubwa umewekwa katika tabia bora za kimaadili kama msingi wa kuimarisha Jumuiya.

Mada na Muktadha Wake

1–35 Sheria na kanuni za haki na usawa kwa ajili ya uendeshaji bora wa maisha ya familia zimewekwa kwa mume na mke. Maelekezo ya kina yametolewa kuhusu mgawanyo wa urithi, na haki za yatima zimezingatiwa kwa makini.

36-42 Ili kufundisha mwelekeo sahihi wa kufuata sheria na kanuni, Waislamu wameamriwa kuonyesha ukarimu kwa wote wanaowazunguka na kujiepusha na uchoyo, ubinafsi, na ubakhili wa akili. Hii ni muhimu kwa uimarishaji wa Jumuiya na kusaidia katika uenezaji wa Uislamu.

43  Njia za kujita­kasa kimwili na kiakili kwa ajili ya kuswali zimefundishwa, kwa kuwa Swla inachukua nafasi muhimu zaidi katika kila mpango wa mageuzi ya maadili na kijamii.

44-57 Baada ya maandalizi ya maadili, maelekezo ya ulinzi yametolewa. Kwanza kabisa, Waislamu wameonywa wajihadhari na hila za ujanja na matendo maovu ya Wayahudi wa eneo hilo ambao walikuwa maadui wa Harakati Mpya. Tahadhari hii ilikuwa muhimu kwa ajili ya kuondoa kutokuelewana ambako kungeweza kutokea kutokana na uhusiano wa zamani kati ya koo za Al-Madina na Wayahudi kabla ya Uislamu. 

58–72 Wameamriwa kuweka amana na majukumu ya uaminifu chini ya ulinzi wa watu waaminifu na wenye sifa, kufanya yaliyo ya haki, na kumtii Mwenyezi Mungu, Mtume wake, na wale waliokabidhiwa jukumu la uongozi miongoni mwao. Pia wamehimizwa kuendesha mambo yao kwa usawa na kumgeukia Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa ajili ya utatuzi wa migogoro. Kwa kuwa mtazamo na mwenendo huu pekee unaweza kuhakikisha uimara wa Jumuiya, wameonywa vikali kwamba kupotoka kokote kutoka katika njia hii kutasababisha kuvunjika kwao.

73-100 Baada ya sharti hili la awali, wamehimizwa kufanya maandalizi ya ulinzi na kupigana kwa ujasiri kwa ajili ya Uislamu, bila kuonyesha aina yoyote ya woga au udhaifu. Pia wameonywa wajihadhari na wanafiki. Mstari wa mipaka umechorwa ili kutofautisha waasi wa makusudi na waumini wasiojiweza. 

101–103 Maagizo yametolewa kuhusu kuswali wakati wa kampeni za kijeshi na mapigano halisi. Hii ni kusisitiza umuhimu wa Swala hata katika mazingira ya hofu na hatari.

104 Kabla ya kuendelea na mada inayofuata, Waislamu wamehimizwa kuendelea katika mapambano yao bila kuonyesha Udhaifu wowote. 

105–135 Ili kuifanya Jumuiya ya Kiislamu iwe thabiti kwa ajili ya ulinzi, Waislamu wameamriwa kuzingatia kiwango cha juu cha uadilifu. Wanatakiwa kutoa haki kwa usawa hata kwa adui anayepambana nao vitani. Pia wanapaswa kutatua migogoro ya kifamilia, hususan kati ya mume na mke, kwa uadilifu. Ili kuhakikisha hili, imani na matendo yao yanapaswa kuwa huru kabisa kutokana na kila aina ya uchafu, na wao wenyewe wawe wabebaji bendera wa uadilifu.

136-175 Wakirudia mada ya utetezi, Waislamu wameonywa kuwa macho dhidi ya maadui zao. Wameonywa kuchukua tahadhari muhimu dhidi ya hila za wanafiki, makafiri na watu wa Kitabu. Kwa kuwa imani katika Mwenyezi Mungu, wahyi wake, na Maisha baada ya kifo ndiyo kinga pekee dhidi ya kila aina ya adui, wanapaswa kumwamini na kumfuata Mtume Wake, Muhammad (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake). 

176 Ingawa aya hii pia inashughulikia sheria za familia zilizomo katika aya ya 1-35, imeongezwa kama nyongeza mwishoni mwa Sura hii kwa sababu iliteremshwa muda mrefu baada ya An-Nisa kusomwa kama Sura kamili.