Aya
18
Mahali iliteremshwa
Madina
SURAT ATTAGHAABUN
(Imeteremka Madina)
Imeanzia Sura hii kwa kueleza kuwa kila kiliomo katika mbingu na katika ardhi kinamtakasa Mwenyezi Mungu na kisio laiki na utukufu wake, na kwamba Yeye ndiye Mwenye Ufalme na Mwenye sifa njema zote, na kwamba Yeye ni Muweza wa kila kitu. Kisha hayo yakafuatilizwa kutajwa baadhi ya dalili za utimilivu wa uweza wake na ujuzi wake. Kisha Sura ikatupa macho kuwaangalia makafiri walio kabla ya hawa, na wakawaasi Mitume na Mola Mlezi, na kwamba wao walionja matokeo maovu ya vitendo vyao. Na hayo yalikuwa hivyo kwa sababu Mitume wao walipo kuwa wakiwajia kwa hoja, waliwakataa na wakawapuuza!
Sura tena ikaingia baada ya hayo kuvunja madai ya makafiri kwamba wao ati hawatafufuliwa. Na ikawataka watu wamuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Nuru iliyo teremshwa juu yake. Na ikawahadharisha na Siku ya Mkusanyo, siku kutapo dhihiri kupunjana kwa watu. Kwani wale walio amini na wakatenda mema watapata kufuzu kukubwa, na walio kufuru ndio watakuwa watu wa Motoni, na hayo ndiyo marudio maovu. Na hakika masaibu yatakuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na hakiki mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu ndio anauongoa moyo wake.
Sura inawataka watu wamtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wakipuuza, basi hakika Mtume hana juu yake ila kufikisha Ujumbe. Na inawaambia Waumini kuwa mali yao na watoto wao ni fitna, majaribio. Basi isiwe kuyashughulikia hayo kukawapelekea kuacha waliyo amrishwa. Kisha ikawaamrisha wamche Mwenyezi Mungu kwa kadri wawezavyo. Na Sura ikakhitimisha kwa kuwakhusisha Waumini watoe katika nia za kheri, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushukuru, Mpole, Mjuzi wa yaliyo fichikana na yanayo onekana. Basi atawalipa kwa mali yao wanayo yatumia. Na kwamba Yeye ni Mwenye nguvu asiye shindilka, Mwenye hikima hafanyi upuuzi.