Aya
53
Mahali iliteremshwa
Makka
SURAT ASH-SHUURA
(Imeteremka Makka)
Hi ni Sura ya Makka, na idadi ya Aya zake ni 53. na imeitwa Ash-shuura, yaani "Kushauriana" kwa sababu inavyo waongoza Waumini waendeshe mambo ya jamii zao kwa kushauriana, ili ipatikane Haki, na uthibiti uadilifu. Na Sura hii imekusanya mambo mengi ya Dini na hoja za itikadi.
Imefungua Sura kwa kuisifu Qur'ani yenyewe kwa kuwa ni Wahyi (Ufunuo) ulio toka kwa Mwenyezi Mungu, ikayarudisha matusi ya makafiri, na ikashughulikia kumpoza Mtume s.a.w, na tena baada ya hayo ikaingilia kuthibitisha uweza wa Mwenyezi Mungu aliye iteremsha Qur'ani na ukatukuka utawala wake, na ikaeleza kukanya kwa baadhi ya watu juu ya kuwa hoja zake ziwazi zinazo onyesha kuwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kubainisha khitilafu zao katika kufahamu Haki. Na baada yake Sura hii ikatilia mkazo uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya kila kitu. Kisha kuwa msingi wa sharia ni mmoja, na ikaashiria kuwa wapo wanao kufuru ikathibitisha juu ya hivyo.
Hali kadhaalika imeashiria kuwa Vitabu vyote vya mbinguni vinaongoza kwendea Haki. Na Sura imelaani shirki ya washirikina, na kukhitalifiana kwao katika Haki kwa udhalimu tu. Na pia imelaani kule kuhimiza kwao, wanao kadhibisha, kuhimiza Kiyama kwa maskhara. Na ikatoa uwongozi kwa wafuasi wake wawalinganie watu kwenye Dini, kama ilivyo eleza ubora wa upole wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Na Sura hii imehadharisha kuzama katika kuiwania dunia tu peke yake. Na ikabainisha uovu wa hali ya makafiri na wema wa hali ya Waumini katika Akhera. Na Sura ikawalaumu wale walio mkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. kwa kumwambia kaizua Qur'ani, hali wao wameshindwa hata kuleta Sura moja tu mfano wake. Kisha ikatangaza kuwa Mwenyezi Mungu ameikubali toba ya Waumini, na ikatangaza hikima ya kuzigawa riziki kwa watu kwa mpango wa hikima. Hawakuwa wote matajiri, kwa kuchelea wasipande jeuri, wala wasiwe wote mafakiri wakateketea. Bali amewakunjulia baadhi na amewadhikisha wengine.
Na akadhihirisha baraka za mvua, na dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu kwa jambo hili. na kwamba masaibu ya dunia ni kwa sababu ya maasi. Kisha Subhanahu akakariri kwa njia nyingine hali za Waumini na wanao kadhibisha huko Akhera, na madhila yatayo wapata wanao kadhibisha. Na akataka wafanye haraka kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu kabla uhai haujakata fursa ya kutenda. Kadhaalika Sura imeshughulika kumpoza Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a. w. na kubainisha uweza wake Subhanahu kumtunukia amtakaye watoto wa kike, na wa kiume mwenginewe, na mchanganyiko kwa wa tatu, na Mwenyezi Mungu kusema na Manabii wake, na ikakhitimisha kwa kubainisha Njia ya kumnyima kabisa wa nne. Kisha Sura ikataja njia za Haki iliyo Nyooka ambayo inayo pasa kuifuata.