Aya
14
Mahali iliteremshwa
Madina
SURAT ASS'AF
(Imeteremka Madina)
Sura hii imefunguka kwa kutoa khabari kwamba viliomo katika mbingu na katika ardhi vinamsabihi Mwenyezi Mungu. Na kwamba haiwaelekei Waumini kusema wasiyo yatenda. Na hakika Mwenyezi Mungu anapenda wawe mkono mmoja.
Kisha Sura imewashutumu Wana wa Israili kuwa ni wenye inda na ukafiri kwa kauli za Mitume wawili watukufu, nao ni Musa na Isa s.a.w. Na kwamba wao wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuitimiza nuru yake. Na ndani ya hii Sura ipo ahadi ya Mwenyezi Mungu - na ahadi yake ni ya kweli - kuwa ataifanya Dini hii ishinde dini zote nyenginezo, hata walau washirikina wakichukia. Na ikakhitimishia kwa kuhimiza Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa hali na mali na kuwaahidi wenye kupigana Jihadi, Mujahidina, kupata msamaha na Pepo, na mengineyo wayapendayo Waumini, nayo ni msaada utokao kwa Mwenyezi Mungu, na ushindi wa karibu. Na wanahimizwa Waumini wawe wenye kumsaidia Mwenyezi Mungu, kama walivyo kuwa wanafunzi wa Isa bin Mariamu. Na kwamba Mwenyezi Mungu atawaunga mkono waumini kwa msaada wake, na Yeye ni Mwenye kushinda katika kila kitu, Mwenye hikima ya ukomo.