Sura Sad

Aya

88

Mahali iliteremshwa

Makka

SURAT S'AAD 

(Imeteremka Makka) 

Sura hii ni ya thalathini na nane katika sura za Qur'ani Tukufu. Nayo ni Sura ya Makka, na Aya zake ni 88. 

Sura hii inatueleza namna ya inda ya washirikina waliyo kuwa wakiufanyia Wito wa Nabi Muhammad sa.w. na uhasidi wao kwa vile Mwenyezi Mungu alivyo mkirimu kwa kumpa utukufu wa Utume, na kumteremshia Qur'ani. Basi inawajibu kwa yale mawazo ya uwongo walio mnasibishia nayo. Na mebainisha kwamba yaliyo wapelekea kuupiga vita Wito wake kama wafanyavyo Si lolote ila ni dharau ya uwongo, na kupenda kuleta khitilafu na mgawanyo. Na lau kuwa adhabu ya Mwenyezi Mungu inge wateremkia, msimamo wao kwa Mtume s.a.w. usingeli kuwa hivyo ulivyo. Kisha Mwenyezi Mungu amewapigia mifano ya kaumu zilizo kwisha tangulia, ili wapate kuacha inadi na kuleta dhiki, na ili kumpa moyo Mtume wake s.a.w. kufikisha Wito, na hata ange pata taabu zozote na vitimbi vyovyote vya washirikina kwa ajili yake. Na apate kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema alizo mpa, kama walivyo fanya ndugu zake Manabii na Mitume wengine. Na kutokea na haya, anataja marejeo mema aliyo waandalia Mwenyezi Mungu wachamngu, na maangukio maovu aliyo waandalia wenye kuasi. 

Kisha akawakumbusha yaliyo kuwa baina ya baba yao Adam (AS) na adui yake Iblisi, ili wajue kuwa anayo waitia Iblisi kufanya kiburi kwa kupinga kufwata haki ni tabia katika tabia zake Iblisi. Na kupanda kiburi huku ndiko kulikuwa sababu ya kufukuzwa kwake kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu.

Sura imekhitimisha kwa kueleza vilivyo kazi muhimu ya Mtume s.a.w., nayo ni kufkisha Wito, na kwamba yeye hawataki ujira kwa hayo, na yeye hakujileta nafsi yake. Na Qur'ani si chochote ila ni Ukumbusho kwa walimwengu wote. Na bila ya shaka watakuja jua ukweli wa khabari zake baadae.