Aya
54
Mahali iliteremshwa
Makka
SURAT SABAA
(Imeteremka Makka)
Sura hii imeanzia kwa kumfanya Mwenyezi Mungu pekendiye kustahiki kusifiwa na kuhimidiwa kwa alivyo waneemesha waja wake. Kwani vyote vilioko mbinguni na katika ardhi ni vyake Yeye kwa kuviumba na kuvimiliki. Na Sura inaeleza porojo la makafiri juu ya Saa ya Kiyama, na kukanya kwao kufufuliwa, na kumsingizia Mtume kuwa ni mwongo na mwendawazimu.Na Mwenyezi Mungu Subhanahu anawarejesha kwenye dalili za uweza wake, na anawahadharisha kuwa atawateremshia kama alivyo wateremshia walio kama wao, na ikawameza ardhi, au vikawaangukia vipande kutoka mbinguni. Na anawakumbusha anavyo wafanyia vipenzi vyake. Kama alivyo mlainishia chuma Daudi, na akamtawalisha Sulaiman na akawafanya majini wamtumikie, wakafanya kama alivyo taka, kama mihrabu na masanamu.
Na Daudi na Suleiman waliishukuru neema, na wachache tu katika waja wa Mwenyezi Mungu wanao shukuru. Hayo yakafuatia maelezo ya neema aliyo waneemesha Mwenyezi Mungu watu wa Sabaa, nao wasishukuru. Hao walikuwa na bustani mbili, ya kulia na kushoto, Miji yao ilikuwa imekaribiana, na wakisafiri baina yao kwa amani. Neema ikawatia kiburi, wakataka safari ziwe ndefu zaidi, Mwenyezi Mungu akawalipa anavyo walipa wanao zikataa neema zake. Nao wakatimiza aliyo fikiri Iblisi na wakamfuata. Na yeye hakuwa na madaraka juu yao, lakini hayo yalikuwa ni mtihani tu wapate kutengana baina ya wanao iamini Akhera na wenye shaka nayo.
Kisha Sura ikaingia kuwaeleza hao wanao wafanya kuwa ni miungu kwamba kwa hakika hawana lolote wawezalo. Na inakumbusha Sura kuwa kila mtu ana jukumu la makosa ayatendayo. Na ikathibitisha Ujumbe wote wa Mtume. Na ikataja kuwa washirikina wanaiona Siku ya Kiyama inachelewa. Na hiyo ina wakati wake maalumu.
Na Sura inasimulia kauli ya makafiri katika Qur'ani, na majadiliano baina ya wakuu na wanyonge, na ikaweka mipaka ya kujifakhari kwa mali na wana, na kwamba hayo mali hayamkaribishi mtu kwa Mwenyezi Mungu ila kwa kadri ya manufaa kwa Watu yanayo patikana kutokana na mali hayo. Kwani hayo mali ni milki yake Mwenyezi Mungu. Na Yeye humkunjulia riziki amtakaye na humdhikisha. Na inawekwa wazi sura ya washirikina. Kwani wao walimwabia Mtume wao kwamba yeye anataka kuwazuilia wasiabudu miungu walio kuwa wakiiabudu baba zao. Na wakaisema Qur'ani aliyo teremshiwa kuwa ni uzushi ulio tungwa, na uchawi dhaahiri! Na pia walidai kuwa hawakupewa Vitabu kabla yake, wala hakutumwa Mtume kabla yake. Na hali hakika tuliwatumia walio kabla yao wanao wajua nguvu zao, na utukufu wao, na khabari zao. Na walipo kuwa hawakuitikia Wito tuliwashika kwa kuwaadhibu.
Na Mtume s.a.w. anaamrishwa aeleze wazi ujumbe wake muhimu kwao. Na hili ni kumbusho bila ya kahari. Na wanaamrishwa wamtazame huyu mwenzao. Hana wazimu. wala hataki mali, na Wito wake kwa watu wafuate Haki ni kwa Ufunuo (Wahyi) unao tokana na Mwenyezi Mungu Mtukufu ili wapate amani. Na itakapo kuj Saa ya Kiyama watafazaika, na watakuwa hawana pa kukimbilia, na watakamatwa pahala karibu. Hapo tena ndio watasema: Tumeamini! Yafaa nini tena hapo Imani nao walikwisha kataa kabla yake. Watazuiwa baina yao na wanacho kitamani,kama walivyo fanyiwa walio kuwa mfano wao. Wao wote walikuwa na shaka tupu katika mambo ya Dini.