Sura Muhammad

Aya

38

Mahali iliteremshwa

Madina

SURAT MUH'AMMAD 

(Imeteremka Madina) 

Sura hii imeanza mwanzo wake kubainisha kwamba Mwenyezi Mungu amezibatilisha amali za makafiri kwa kuwa wamefuata upotovu, na amewafutia Waumini maovu yao kwa kufuata kwao Haki. Kama ilivyo eleza kwa urefu waajibu wa kuitetea Haki. Na malipo hayo kwa Akhera ni kuingia Peponi Na ikawahimiza Waumini wainusuru Dini ya Mwenyezi Mungu na wapigane kwa ajili yake. 

Na imeweka wazi kwamba wapotovu wakiacha Imani hufanya fisadi katika nchi na wakawatupa jamaa zao. Na inahadharisha juu ya wanaafiki kuwa pamoja na Waumini wakapeleleza siri zao wapate kuwavunja moyo. Na inawatishia wanaafiki kuwa yatachanwa mapazia yao wanayo jifichia, na Mtume wa Mwenyezi Mungu adhihirishe chuki zao. Na inawakataza Waumini wasiwe wanyonge katika kupambana na makafiri, na hali wao ndio watakao shinda, na Mwenyezi Mungu yu pamoja nao, na wala hatawanyima malipo ya kazi yao. 

Kisha Sura imekhitimisha kutaka watu watoe kwa sababu ya Sabili Llah, Njia ya Mwenyezi Mungu, na ikabainisha kwamba mwenye kufanya ubakhili katika hayo basi anajidhuru mwenyewe, na kwamba kuacha kufuata Haki inakuwa ndiyo sababu ya kuhiliki hao wenye kuacha na kuletwa kaumu nyengine zenye kuleta kheri.