Sura Al-Fajr

Aya

30

Mahali iliteremshwa

Makka

SURAT AL-FAJR 

(Imeteremka Makka)

Imeanza Sura hii kwa viapo vya mambo yanayo onekana namna mbali mbali, yanayo pelekea kuangalia athari ya kudra kwamba wanao mkanya Mwenyezi Mungu na kukanya kufufuliwa watakuja adhibiwa, kama walivyo kwisha adhibiwa walio kadhibisha kabla yao. Na Sura ikaingia kuthibitisha mwendo wa Mwenyezi Mungu wa kuwajaribu waja wake kwa kheri na shari, na kwamba kupa kwake na kunyima kwake sio dalili ya kuridhika kwake au kukasirika kwake. Tena mazungumzo yakawaelekea wanao semezwa ya kwamba hali zao zinafichua wingi wa pupa yao na choyo chao. Kisha inakhitimisha kwa kuashiria majuto ya wanao pindukia kiasi na kutamani kwao kwamba laiti wangeli tanguliza mema ya kuwaokoa na hayo wanayo teseka nayo ya vitisho vya Siku ya Kiyama, na yanayo kuwa ya kuiliwaza nafsi iliyo tua iliyo tanguliza mema wala isikiuke mipaka, na itavyo itwa iingie pamoja na walio kirimiwa miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu katika Pepo ya Mwenyezi Mungu.