Aya
45
Mahali iliteremshwa
Makka
SURAT FAAT'IR
(Imeteremka Makka)
Sura hii imefunguliwa kwa kumsifu Mwenyezi Mungu, Muumba mbingu na ardhi, bila ya ruwaza. Mwenye kuwafanya Malaika kuwa ni wajumbe wa kuwatuma kwa waja wake. Malaika hao wana mbawa za idadi namna mbali mbali. Fadhila yoyote anayo wapelekea watu hapana wa kuizuia; na anayo izuia hapana wa kuipeleka. Mwenyezi Mungu anawataka watu waikumbuke neema, kwani hapana muumba mwengine aliye pamoja naye wa kuwapa riziki, wala hapana mungu pamoja naye wa wao kumwendea. Na watu wamekanusha wito wako. Lakini wewe unayo mazingatio kwa yaliyo wapitia Mitume walio tangulia. Nawe unayo ya kukuliwaza kwa tulivyo ahidi kuwa watarejea kwetu.
Na waajibu kwa watu wasidanganyike na dunia na mapambo yake. Na asiwadanganye Shetani. Na shauri yake ni fupi, haipindukii kuliko kuwapelekea hao wafwasi wake kwenye maangamizo. Na mwenye kumfuata atamwongoza ampeleke Motoni. Wala hawawi sawa, mwenye kumpambia Shetani vitendo vyake viovu, na aliye muacha. Ilivyo kuwa shani ya watu ni hiyo, basi usisikitike kwa kuto amini kwao. Kwani Mwenye kuyapeleka mawingu na akahuisha kwayo kilicho kufa, atawafufua wafu kwa ajili ya hisabu na malipo. Mwenye kutaka nguvu atafute nguvu kwa Mwenyezi Mungu. Na mwenye kutafuta nguvu kwa mwenginewe, atamdhalilisha. Na vitendo vya waja vinapanda kwendea kwake. Yeye, basi huvikubali vitendo vya Waumini, na huviangusha vitendo vya makafiri.
Na dalili ya uweza wake kufufua na kukusanya Siku ya Kiyama, ni kuwa kamuumba mwanaadamu kutokana na udongo kisha kutokana na tone la manii, tena akawafanya mwanamume na mwanamke. Wala mwanamke hachukui mimba wala hazai ila kwa ujuzi wake. Ameumba utamu na chumvi, na katika vyote hivyo unapata riziki. Na akauingiza usiku katika mchana, na mchana katika usiku. Na akafanya jua na mwezi yatii, kila kimoja wapo kinakwenda kwa muda maalumu. Muweza huyu ndiye Mungu wa Haki. Na hao wanao waomba badala yake hawamiliki, na wakiitwa hawasikii, na wakisikia hawajibu. Na Siku ya Kiyama hao wataukataa ushirikina walio washirikisha na Mwenyezi Mungu. Na Yeye ni Muadilifu, anambebesha kila mtu a'mali yake. Na wanaelekezwa Mitume wawakusudie kwa wito wao wale wanao mwogopa Mwenyezi Mungu. Na kazi ya Mtume ni kuwaonya watu wake. Na hapana umma wowote ila ulipitiwa na Mwonyaji.
Sura tena inarejea kwenye dalili za uweza, kudra ya Mwenyezi Mungu. Kwa maji yanatokea mazao ya kila namna, na katika mawe ya majabali yapo namna mbali mbali, nyeupe, nyekundu na nyeusi. Na watu na wanyama pia zinakhitalifiana rang zao. Yote hayo yanapelekea kumnyenyckea Mwenyezi Mungu. Na mwenye kusoma kitabu cha Mwenyezi Mungu alicho mrithisha aliye mteuwa ataingia Peponi astarehe humo. Na mwenye kukufuru ataingia Motoni, hakuna mwisho huko, wala kupunguziwa adhabu yake. Atataka arejezwe duniani ili atengeneze vitendo vyake, naye alikwisha pewa muhula wa kukumbuka lau kuwa ni mwenye kukumbuka. Na aliwajia Mwonyaji. Na Yeye, Subhanahu amekufanyeni ni warithi wa walio tangulia katika ardhi. Naye anaizuia mbingu isiondoke: Na wenye inadi waliapa kwamba akiwajia Mwonyaji hapana shaka watakuwa waongofu zaidi kuliko walio watangulia.
Alipo wajia wakatakabari, basi vitimbi vyao vikawaangukia wenyewe. Na wao hawakumkadiria Mwenyezi Mungu anavyo stahiki kukadiriwa. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wachukulia watu wa duniani kwa wanayo yafanya asingeli mwacha mnyama yoyote. Lakini anaakhirisha mpaka muda wao. Ukifika basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake.