Aya
59
Mahali iliteremshwa
Makka
SURAT ADDUKHAN
(Imeteremka Makka)
Sura hii imeanza kwa kusimulia khabari za Qur’ani, ya kwamba imeteremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika usiku wa Lailatul Qadri ulio barikiwa, kwa ajili ya kuonya na Tawhid, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja. Na kwamba hii Qur'ani ni Haki, Kweli tupu. Hali kadhaalika Sura imesimulia khabari za kufufuliwa, na kwamba hayo hayana shaka ndani yake, na imezibisha hoja za wanao yakanya hayo, na ikawarudi washirikina. Ikalinganisha baina ya washirikina wa Makka na wenzao walio watangulia, nao ni kaumu ya Firauni. Ikaeleza mapatilizo ya Mwenyezi Mungu yaliyo washukia hao.
Tena ikatilia mkazo kwamba Siku ya Kiyama ndiyo siku iliyo pangwa ya kuutenga ukafiri na upotovu wote. Na ikasimulia malipo ya wakosefu kwa siku hiyo na malipo ya walio ongoka. Na ikamalizika kama ilivyo anzia kwa mazungumzo juu ya Qur'ani, na kwa kuwaonya wanao kadhibisha Ujumbe wa Mtume s.a.w. kuwa nao wangojee balaa na masaibu yatakayo washukia.