Sura Ar-Raad

Aya

43

Mahali iliteremshwa

Madina

SURAT AR-RAA'D 

(Imeteremka Madina)

"Surat Ar Raa'd" ni Sura ya Madina, na imeitwa "Raa'd" kwa kusimuliwa kwamba Radi (inamsabihi) inamtakasa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hisabu za Aya zake ni arubaini na tatu. Imeanza Sura hii kwa kubainisha cheo cha Qur'ani Tukufu, na kwamba imeteremshwa kwa Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. 

Kisha ikabainisha uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika ulimwengu wote, na ikazindua kueleza mambo yaliyo umbwa na yenye manufaa Kisha ikatoka kubainisha uwezo wake Mwenyezi Mungu wa kuumba, ikaingia kubainisha uwezo wake kurejesha tena na kufufua, na ujuzi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu wa kila kitu, na kubainisha kudra yake ya kuadhibu duniani, na kwa hivyo yaweza kukisiwa adhabu ya Akhera. Kisha Sura hii ikaelekeza nadhari zizingatie maajabu ya ulimwengu yaliyo zagaa. Baada ya hayo Mwenyezi Mungu Mtukufi amezieleza hali za watu katika kupokea kwao uwongofu wa Qur'ani. 

Kisha akataja sifa za Waumini katika makhusiano yao ya kibinaadamu, na tabia za makafiri na karaha yao kushikilia kutaka miujiza isiyo kuwa hii Qur'ani juu ya ubora wake wa cheo, na ikataja kejeli zao kwa Mtume wao. Na ikamueleza Mtume kuwa Mitume wa kabla yake pia walifanyiwa kejeli! Na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye kusimamia vitu vyote na nafsi zote, na kwamba Yeye ni Mwenye kumlipa kila mtu kwa anavyo stahiki, na kwamba Qur'ani ndio muujiza mkubwa kabisa utakao baki mpaka Siku ya Kiyama, na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye anaye wapa nguvu Mitume wake kwa miujiza aitakayo. Na ikiwa hao washirikina wanakanya Utume wa Nabii huyu, basi Mwenyezi Munge Mwenyewe anashuhudia ukweli wake, na Yeye ni Mwenye kutosheleza kwa hayo.