Sura An-Nahl

Aya

128

Mahali iliteremshwa

Makka

SUURAT AN NAH'L 

(Imeteremka Makka)

Sura hii ni ya Makka isipo kuwa Aya tatu Za mwisho. Hizo ni Za Madina. Idadi ya Aya zake ni mia na ishirini na nane. Sura hii tukufu imeanzia kutilia mkazo maonyo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwapa washirikina, na kubainisha uwezo wake Subhanahu wa Taa'la katika kutimiza ahadi hiyo, kwa dalili ya kuumba kwake mbingu na ardhi, Kisha kawabainishia watu wote kumuumba kwake ngamia, na kuotesha kwake makulima, na aliyo yaumba baharini, kama Samaki wa kuliwa, na majohari ya mapambo. Kisha akaashiria yanayo wajibikia kwa neema hizo, nayo ni kumshukuru Subhanahu, na waajibu wa kumuabudu Yeye peke yake, na kuwakabili washirikina kwa kuwaita watambue Upweke wa Mwenyezi Mungu; na imetaja uzushi wa washirikina kuizulia Qur'ani Tukufu, na kudai kuwa hiyo ni hadithi za uwongo za kale. 

Kisha Subhanahu ameashiria adhabu ya washirikina Siku ya Kiyama na starehe za Waumini. Baadaye Subhanahu akataja kukanya kwa washirikina kukhusu kufufuliwa na kushikilia kwao kukanya. Naye Subhanahu anapinga ukafiri wao kwa kubainisha uwezo wake, na anatilia mkazo ahadi yake kwa wachamngu na vitisho vyake kwa makafiri. 

Kisha anakaribisha kufufuliwa kwa kueleza uwezo wake juu yao, na kuwa viumbe vyote vinamnyenyekea Yeye Aliye takasika, na anabainisha kuwa ni Yeye Subhanahu ndiye anaye kashifu. Na anabainisha upotovu wa washirikina katika itikadi yao kuamini vitu visivyo weza kuleta nafuu wala madhara, na uovu wa maoni yao kwa wanawake wote, watoto na watu wazima. Naye Subhanahu ameashiria khabari za Mitume walio tangulia, akataka tuuzingatie uumbaji wake wa vitu na faida ziliomo ndani yake kwa ajili ya watu, na kutafautiana riziki kuwa matajiri wanapewa Zaidi kuliko masikini, na neema zake kwa watu kuwa wengine wanaume na wengine wanawake, na kuzaliana kwa kuoana. 

Naye  Subhanahu akaingia kupiga mifano ili kueleza kudra yake. Kisha akataka watu waangalie vipi ubora wa kuumba unavyo onyesha ubora wa Mwenye kuumba na kuenea neema zake. Na vipi washirikina wanavyo zipinga neema hizi tukufu. Na baada ya kueleza matakwa ya Uislamu kuleta uadilifu, na kuunganisha udugu kwa kutimiza ahadi, na muujiza wa Qur'ani, na ukafiri wa washirikina kuikataa Qur'ani, na kuizulia uwongo, Aliye takasika ameashiria hali ya washirikina Siku ya Kiyama. Amebainisha vipi walivyo kuwa wakihalalisha na wakiharimisha bila ya hoja. Akaashiria vipi Mayahudi walivyo wakaribia washirikina na akabainisha kuwa yapasa wasiadhibiwe isipo kuwa kwa kadiri ya walivyo tenda, na kuwa ni waajibu wa Waumini wasubiri, na washikamane uchamngu na kufanya ihsani.