Aya
88
Mahali iliteremshwa
Makka
SURAT AL-QAS'AS'
(Imeteremka Makka)
SURA YA AL-QAS'AS' ni ya 28 katika mpango wa Msahafu. Nayo ni Sura ya Makka. Aya zake ni thamanini na nane.
Imetaja kwa kufafanua yaliyo kwisha tajwa kabla yake kwa jumla katika mambo ya Musa (AS) tangu kuzaliwa kwake katika enzi ya Firauni. Na Firauni alikuwa akiwauwa watoto wanaume wa Bani Israili kwa kukhofu asije tokea Nabii miongoni mwao atakaye teketeza ufalme wake.
Kisha yakaelezwa yaliyo tokea kukhusu kulelewa kwake Musa katika nyumba ya Firauni, mpaka alipo itoka Misri kukimbiza roho yake kwenda Madiani katika nchi ya Shamu. Na tena akarejea na mkewe, binti wa Shuaibu (AS).
Kisha yakatajwa mazungumzo ya Mwenyezi Mungu na Musa, na kumteuwa yeye kwa kumpa Utume, na mambo yaliyo tokea yaliyo mkhusu Firauni na wachawi wake pamoja na Musa, mpaka Mwenyezi Mungu alipo mzamisha Firauni na jeshi lake. Na Musa na Wana wa Israili walio kuwa pamoja naye wakaokoka. Kisha yaliyo watokea Wana wa Israili pamoja na Musa nduguye Harun. Na zimetajwa pia khabari za na walio kadhibisha kama Qaaruni na makafiri wengine walio watangulia. Na kwa maelezo haya yaliyo kusanya khabari mbali mbali ndio Sura hii ikaitwa Surat al- Qas'as', yaani Sura ya Visa, au Hadithi.