Aya
111
Mahali iliteremshwa
Makka
SURA AL ISRAAI (BANI ISRAIL)
(Imeteremka Makka)
Sura hii tukufu ina Aya 111, nayo ni Sura ya Makka ila Aya hizi: 26, 32, 33, 57 na tangu Aya 73 mpaka Aya 80. Aya zote hizi. nazo ni 12, ni za Madina. Sura hii imeanza kwa kumsabihi, kumtakasa, Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kisha ikaitaja Israi, nayo ni safari ya usiku aliyo chukuliwa Mtume s.a.w. kutoka Makka mpaka Bait Al Muqaddas (Yerusalemu), na baadae akapelekwa mbinguni, na kurejeshwa Makka usiku ule ule.
Baadae Sura inaeleza Ujumbe wa Nabii Musa (AS), na yaliyo kuwa ya Wana wa Israili Kisha ikaashiria cheo cha Qur’ani Tukufu katika uwongofu, na zikatajwa Aya za uumbaji usiku na mchana, na yatakayo watokea watu Siku ya Kiyama katika kulipwa kwa vitendo walivyo vitenda duniani. Na Subhanahu amebainisha sababu ze kuharibika umma, na hali ya watu katika kuhangaika kwao, na matokeo ya vitenda vyao huko Akhera. Tena zikaja Aya za kutukuzwa wazazi, baba na mama, na hali ya watu kukhusu mali zao; na zikaja Amri Kumi za kuunda umma ulio bora. Kisha Subhanahu akauvunja uzushi wa washirikina kukhusu Malaika, kisha akabainisha Qur'ani inavyo eleza hoja zake.
Kisha Subhanahu akaashiria anavyo stahiki kuhimidiwa, na upinzani wa washirikina, akawapa wasia Waumini. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akaeleza namna anavyo watendea makafiri duniani na Akhera. Tena akaeleza asili ya uumbaji wa binaadamu na Shetani, na akawatisha washirikina kwa Aya zake. Baada ya hayo, Subhanahu alibainisha utukufu wa binaadamu, na akataja adhabu za Siku ya Kiyama. Akataja vipi washirikina wanavyo jaribu kumzuia Nabi asitimize Wito wake, na vipi Mwenyezi Mungu anavyomtia nguvu. Baada ya hayo Allahu Subhanahu wa Taa'la akamuusia Nabii kwa wasia za uwongofu, na wito mnasaba. Kisha akaashiria cheo cha Qur`ani Tukufu. na akataja khabari za Roho, na akaashiria siri zake. Kisha akataja umuujiza wa Qur'ani, kushindwa majini na watu kuleta mfano wake. Na akabainisha Subhanahu uwezo wake kuleta Ishara nyengine. Tena akataja vipi Qur’ani ilivyo kusanya Haki; na hali za Waumini wema katika Imani zao, na inavyo takikana kuwa daima wawe wanamhimidi Mwenyezi Mungu na wakimtukuza.