Sura Al-Anfal

Aya

75

Mahali iliteremshwa

Madina

SURAT AL ANFAAL 

(Imeteremka Madina) 

Surat Al Anfaal hii imeteremka Madina. Aya zake ni 75. Mwenyezi Mungu aliye takasika na kutukuka, amebainisha katika Sura hii baadhi ya hukumu za vita, na mambo yanayo pelekea vita, na sababu za ushindi, na makamo ya nguvu za moyo zinazo pelekea kushinda, na hukumu za ngawira za vita, na wakati gani kuchukua mateka. 

Na Mwenyezi Mungu kwa hikima yake amekusanya humu hukumu za kisharia. Sura hii inaeleza kisa cha Vita vya Badri, na baadhi ya yaliyo kuwa kabla yake, na kuashiria sababu zilizo sabibisha hivyo vita, nazo ni kutoka makafiri washirikina Makka kumwendea Nabii s.a.w. Na humu Mwenyezi Mungu anataja ujitayarisha kwa vita, na kupasa kuelekea salama na amani ikiwa maadui wanaelekea kutaka salama. 

Na Sura hii tukufu inamalizikia kubainisha urafiki wa Waumini, wao kwa wao; na kuwawajibikia Waumini kuihama nchi inayo waonea na kuwafanya wanyonge, ili wende kuwaunga mkono Waumini wenzao katika juhudi ya kutukuza Uislamu na Waislamu.