Sura Al-Ahzab

Aya

73

Mahali iliteremshwa

Madina

SURAT AL-AH'ZAB 

(Imeteremka Madina)

Sura hii imeanza kwa kumtaka Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. amche Mwenyezi Mungu na amtegemee Yeye. Tena ikaingia kuzungumza juu ya mas-ala ya watoto wa kupanga na ikakataa kuwa hao wana wanao walea kuwa ni watoto wao khasa. Na  ikataja mapenzi na utiifu wa Mwenyezi Mungu alio wajibisha kwa ajili ya Mtume wake, na hishima na kuwatukuza Mamama wa Waumini, yaani wake za Mtume. Na  Sura imeeleza ahadi aliyo ichukua Mwenyezi Mungu kwa Manabii kuwa wafikishe ujumbe; na ikafafanua khabari za Vita vya Ah'zab (Makundi) na khofu na misukosuko iliyo kuwako, na vipi mwishoe Waumini wakashinda na ahadi ya Mwenyezi Mungu ikatimia. 

Na Sura hii ikashughulikia kutaja adabu ambazo zinawapasa wake za Mtume kuzifuata, na wajilazimishe nafsi zao kuzishika. Tena ikaangukia kuzungumza juu ya watoto wa kupanga. Na ikavunja ada ya siku za kijahiliya, za ujinga, ilipo kuwa  kuharimisha mtu kuoana na mwana wa kupanga ambaye kwa hakika ni halali yake. Na Sura ikamsifu Mtume s.a.w. na ikamthibitishia aliyo kuwa anastahiki. Na ikausia kustareheshwa na kumwacha kwa wema mwanamke anaye pewa talaka kabla ya kuingia harusi. Na ikamkhusisha Mtume s.a.w. kuwa imemhalalishia mwanamke aliye jitolea kuolewa naye, na ikasema wazi kuwa si halali kwake kuzidisha kuowa wanawake wengine baada ya hao tisa alio kuwa nao. 

Kisha Sura tukufu ikabainisha yanayo wajibikia Waumini kuyafuata wanapo ingia nyumba za Nabii kwa ajili ya kula na kuwa wakisha wende zao, na juu ya kuwauliza wake zake nyuma ya pazia. Na Sura ikawataka Mamama wa Waumini (wake za Mtume s.a.w.) wateremshe mitandio yao juu ya vifua yao. Na Sura ikazungumza juu ya Saa na vitisho vya Kiyama, na ikatoa nasaha ya kumcha Mwenyez Mungu, na kusema maneno yaliyo sawa, na ikakhítimishia kwa kutaja jukumu la Mwenyezi Mungu alilo libeba mwanaadamu, hali mbingu na ardhi na milima ilishindwa kulibeba.

Kutokana na hayo inaonekana kuwa makusudio muhimu kabisa ya Sura hii ni Maneno Juu ya watoto wa kupanga, na kuivunja ada iliyo kuwa imeenea wakati ule kuharimisha kuwaoa wana wa kupanga ambao ni halali kwao; na ihsani ya Mwenyezi  Mungu kuwafanyia Waumini kwa ushindi kuwashinda washirikina kama alivyo waahidi; na kufafanua sharia aliyo wawekea Mwenyezi Mungu Waumini wanapo ingia nyumba za Nabi s.a.w. ma kuwaharimishia kuwaoa wake zake baada yake, na kuzipanga adabu makhsusi zilizo wakhusu Mamama  wa Waumini, yaani wake za Mtume s.a.w.